| Intro | Tanzanian political leader and poet |
| Is |
Politician Poet |
| From | Tanzania |
| Type |
Literature Politics |
| Gender | male |
| Birth |
8 December 1926, Ujiji, Tanzania |
| Age | 94 years |
| Star sign | Sagittarius |
| Politics | Tanganyika African National Union |
Saadani Abdu Kandoro (alizaliwa katika eneo la Kasingirima-Ujiji mkoani Kigoma tarehe 8 Desemba 1926) alikuwa mwanasiasa na mshairi nchini Tanzania. Anahesabiwa kati ya wanasiasa waliopigania uhuru wa Tanganyika wakishirikiana na Julius Nyerere.
Maisha
Baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi Ujiji alijiunga na shule ya upili ya serikali huko Iringa na baadaye Chuo cha Ualimu cha Bwiru, Mwanza.
Mwaka 1944 aliingia katika utumushi wa serikali ya kikoloni kwenye idara ya kuweka hazina Uyui Tabora.
Aliendelea kujishughulisha na katika kuanzisha vyama vya ushirika na hatimae akawa diwani wa Advisory Coucil ya mji wa Tabora .
Tangu 1940 alishiriki katika Tanganyika African Association (TAA).
Mnamo mwaka 1954 alikuwa miongoni mwa watu 17 walioanzisha chama cha TANU mjini Dar es Salaam.
Ilipofika mwaka 1962, aliteuliwa kuwa katibu wa TANU na kamishna wa wilaya ya Mafia. Mwaka 1964 aliendelea kuwa katibu wilaya ya Mafia ambapo alihudumu hadi mwaka 1970 ambapo aliacha kazi hiyo na kuamua kujishughulisha na ukulima.
Mashairi
Pamoja na Ushairi na siasa, Saadani A. Kandoro amendika mashairi mengi ya malumbano akipambana na magwiji wa ushairi na wanasiasa wakubwa wa Tanzania akiwemo mwalimu Julius Nyerere.
Shairi hili aliandikiwa na Mwalimu Nyerere kama ujumbe:
Sheikh Kandoro sikia
1. Sheria husaidia
Kuijenga Tanzania
Siyo kazi ya sheria
Nchi kutuharibia.
2. Kila nchi ina nia
Inayoikusudia
Vilevile ina njia
Itakayoipitia.
3. Tanzania tuna nia
Ya kujenga ujamia
Na njia ya kupitia
Ni wote kusaidia.
4. Kijiji chaturadhia
Kisima kujipatia
Lamgambo limelia
Watu wakahudhuria.
5. Wakakubali kwa nia
Kisima kujichimbia
Aliye wakatalia
Kukuye wakamlia.
6. Akaenda kushtakia
Kwa hakimu wa sheria
Kwamba wamemuonea
Kuku wake kumlia.
7. Hakimu akasikia
Akaita jumuia
Wakaja akawambia
Nyinyi mwavunja sheria.
8) Basi nawahukumia
Faini shilingi mia
Na sabini za fidia
Au jela kuingia.
9) Hakimi wakamwambia
Itatushinda fidia
Hata na faini pia
Heri jela kuingia.
10. Wakafungwa kwa sheria
Na maji wakamwachia
Mwenye kuku kuumia
Pamwe na hakimu pia.
11. Huko ni kusaidia
Adui wa jummuia
Nasi kazi za sheria
Ila ya maharamia.
12. Kazi hasa ya sheria
Kusaidia raia
Si nia kuwavunjia
Wanapojisaidia.
Saadani Kandoro aliandika shairi lifuatalo kumjibu Mwalimu Julius Nyerere:
1. Labeka muheshimiwa
Julius msifiwa
Kambarage muelewa
Bwana nakuitikia.
2. Nakuitikia sheria
Kwamba inasaidia
Kuijenga Tanzania
Na ni nguzo ya dunia.
3. Kutoheshimu sheria
Huleta wingi udhia
Amani ikapotea
Nchi zikaangamia
4. Ni msumeno sheria
Methali hii natia
Haitaki kubabia
Pendeleo liso njia.
5. La mgambo likilia
Watu wote hudhuria
Kisima kujichimbia
Hilo lataka sheria.
6. Kuna wavivu wa nia
La mgambo likilia
Nao wanajikalia
Haendikuhudhuria.
7. Mfano huo hatua
Wengine hufuatia
Na wao hujikalia
Kazi zetu husinzia.
8. Kimila nimesikia
Waweza kumfikia
Kuku wake kujilia
Lakini siyo sheria.
9. Kwa kuwa siyo sheria
Mvivu kujistakia
Na walao huumia
Pia huyozwa fidia
10. Twazidi kukulilia
Lifanywe hasa sheria
By law kujitia
Naweza kusaidia.
11. Yaweza kusaidia
Kuku tukijilia
Pasiwepo hata njia
Mvivu kukimbilia.
12. Kuku tumejilia
Pasiwe la kuponyea
Hakimu kumuendea
Kwamba ilipwe fidia.
13. Mkwazo twaukazia
Bila nyuma kurudia
Twataka kuendelea
Kuinuwa Tanzania.
14. Taifa kuitikia
Kazi kuzishangilia
Ndio tunalo Lilia
Ndipo tunakazania
15. Ndipo tunakazania
Na tena tunakania
Kuishangaza dunia
Lengo letu kutimia.
16. Bila nguvu kuzitia
Mkazo wa kisharia
Unafaa kufutia
Kazi zikaendelea.
Mbali na Mwalimu Nyerere, Kandoro pia walikuwa akiandikiana mashairi na washairi wakubwa huku akishindana na magwiji hapo kama kina Moses Mnyampala, Salahe Kibwana, Mdanzi Hanasa na wengine wengi.
Alifanikiwa kutoa kitabu maarufu “Mashairi ya Saadani” ambacho kilichapishwa na Shirika la Magazeti ya Chama Ltd.
Tanbihi
Marejeo ya Nje
- Kandoro, Saadani Abdu 1926- , vitabu vyake kwenye WorldCat
| Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Saadani Abdu Kandoro kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |